Saturday, July 23, 2011

Kashfa ya IPTL kama Rada II
Joseph Mihangwa
29 Jun 2011
Toleo na 192
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii, tuliona jinsi mkataba wa miaka 20 wa kuuziana umeme [PPA] ulivyofikiwa kati ya IPTL na TANESCO, mkataba ambao umeitupa nchi yetu gizani kwa mgawo wa umeme wakati serikali itaendelea kuilipa IPTL zaidi ya Sh. bilioni 6 kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo kwa kipindi chote hicho.
Tamko la serikali kupitia kwa Waziri wa Madini na Nishati, William Ngereja, hivi karibuni kwamba tatizo la umeme nchini litamalizika mwaka 2015, linakwenda sambamba na muda wa mkataba huo wa IPTL wa miaka 20 [kuanzia 1995] utakapomalizika mwaka huo.
Tuliona chimbuko la mkataba huo wa kifisadi, kuanzia na ziara ya Waziri wa Mipango wa wakati huo, hayati Horace Kolimba nchini Malaysia, Julai 1994, alikozungumza na wawekezaji katika sekta ya umeme wa nchi hiyo na kuwaomba waje nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza ili kupunguza tatizo la umeme.
Agosti 19, mwaka huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mechmar, inayomiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL, Bw. Datuk Baharuden Majid, aliongoza ujumbe mzito kutoka Malaysia kuja kufanya mazungumzo na serikali yetu juu ya uwekezaji huo. Walioshiriki katika mazungumzo hayo kwa niaba ya serikali yetu ni pamoja na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa wakati huo [na sasa Rais wa Tanzania], Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Simon Mhaville, Kamishna wa Nishati Msaidizi, Ester Masunzu, na Msaidizi wa Rais Ali Hassan Mwinyi wa Mambo ya Uchumi, Dakta Juma Ngasongwa.
Viongozi na watendaji hao wakuu wa serikali, kwa nia njema na thabiti kabisa, waliukaribisha uwekezaji huo bila kujua kwamba hatimaye ungeingiliwa na “dumuzi” mharibifu; kwa maana ya ufisadi kwa njia na mtindo ule ule uliotumika kwa kashfa ya rada.
Mwezi mmoja baadaye, Septemba 1994, Mkataba wa Maelewano [MOU] ulifikiwa baada ya kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa nchi, kuwa ulikuwa mzuri na wa manufaa kwa nchi; licha ya tahadhari kutoka kwa washauriwa wa TANESCO – Kampuni za Acres [Canada] na Hunton and Williams [UK], kwamba uwekezaji huo ulikuwa hati ya kifo kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa Taifa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, ufisadi mwingi na mkubwa wa kutisha kwa uchumi wa nchi, mara nyingi umefanyika karibu na chaguzi kuu hasa katika enzi hizi za demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Mfano hai ni pamoja na kashfa za Meremeta, EPA, Richmond/Dowans na nyinginezo, ambapo mabilioni ya fedha jasho la wananchi, yameporwa bila huruma na mikataba mibovu kuingiwa kwa kisingizio cha “usalama”, “ustawi” au “manufaa” ya Taifa, wakati ukweli ni kinyume chake. Mkataba wa IPTL unaweza kuwa mmoja ya mbinu hizo.
Tunafahamu kwamba, mazungumzo juu ya uwekezaji huo yalianza mwaka 1994 kwa ziara nchini Malaysia ya Waziri wa Mipango na Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, hayati Horace Kolimba na hatimaye makubaliano kufikiwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.
Ni katika kipindi hicho, kigogo mmoja wa Chama [Dakta Abdallah Kigoda] aliyekuwa na cheo cha chini tu kwenye Tume ya Mipango ya Taifa, aliteuliwa kuwa Mtunza Hazina wa CCM, na hivyo kuingia katika “gurudumu” la Chama tawala.
Alipotembelea Malaysia, kigogo huyo alirejea nchini na “kitita” cha fedha kwa ajili ya kugharamia mkutano muhimu wa CCM, ingawa fedha zilizotumika na jinsi zilivyotumika zilizua malumbano na utata miaka miwili tu baadaye.
Mwafaka tata na tete
Baada tu ya kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Ujenzi [EPC] mwaka 1997, alipanda cheo ghafla kuwa Waziri wa Wizara nyeti yenye dhamana ya sekta ya umeme nchini. Ni mwafaka gani huo wenye matukio tata na tete yenye kushabihiana?
Ufisadi katika mradi huu ulianza kujidhihirisha mwezi Februari, 1995 katika ununuzi wa mitambo ya mradi. Awali, Kampuni ya Wartsila ilikuwa imeomba kuuza jenerata za kufua umeme 11 aina ya Slow Speed Diesel [SSD] zenye uwezo wa kuzalisha megawati 116 za umeme kwa bei ya dola milioni 53 tu pamoja na vifaa vyote.
Lakini Februari 15, 1995 bei ya jenereta hizo iliongezwa kinyemela kufikia dola milioni 85.7, na dola milioni 114.2, Januari 1996, na hatimaye dola milioni 163.5 kwa gharama za ujenzi [EPC] na dola milioni 126.39 kwa jenereta 10 tu.
Nyumba 37 zilizopangwa kujengwa pale Tegeta zilipunguzwa kutoka 37 hadi 6, lakini kwa gharama ile ile ya nyumba 37 kwa dola milioni 7.6!
Kuna ushahidi kuonyesha kwamba, kampuni hiyo hiyo Wartsila, iliziuzia nchi nyingine za Kiafrika, ikiwamo Kenya, Jenereta kama hizo za Mradi wa IPTL, kwa chini ya dola milioni 60. Na kama kwamba hiyo haikutosha, IPTL ilibadili mitambo SSD na kusimika mitambo hafifu na ya bei ya chini zaidi lakini ya aghali kuendesha, aina ya Medium Speed Diesel [MSD] kwa bei ile ile ya SSD, ili kujipatia kivuno kwa kupora kutokana na tofauti ya bei kinyume na mkataba, na bila TANESCO kujua.
Kwa hiyo, ukichukulia kwamba nchi yetu iliuziwa mtambo mbovu kwa bei mbaya; ukichukulia pia kwamba mradi huo uliongezwa gharama kinyemela kwa asilimia 130 badala ya gharama halisia; na ukichukulia zaidi kwamba mkataba huo wa kitapeli umeifanya Serikali yetu kulipa zaidi ya Sh. bilioni 6 kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo na nchi kuingia gizani; hivyo kwa njia hii, ufisadi wa IPTL umetwisha mzigo uchumi wa nchi na kuturudisha nyuma hatua tatu katika maendeleo.
Wananchi walonga kuhusu mkataba
Wananchi nao hawakukaa kimya juu ya sakata hili kati ya IPTL na TANESCO. Mmoja wa wananchi walioonyesha kukerwa ni Brigedia Jenerali mstaafu, Joachim Burcard Ngonyani aliposema: “Hebu angalia mkataba wa IPTL; ni mkataba wa kihayawani kweli kweli. Tunataka wote waliouidhinisha washughulikiwe. Uchu wao wa kujilimbikizia mali usiruhusiwe kudidimiza uchumi wa nchi hii” [The African, August 3, 1996].
Naye Mbunge wa Dodoma mjini wa wakati huo, Mheshimiwa Hashim Saggaf, alishangaa kuona kwamba waliotia sahihi mkataba huo hawajahojiwa na serikali ili waeleze kwa nini wametufikisha hapo [The East African, April 26, 1999].
Inaelekea kila mtu alielewa mchezo mchafu uliochezwa na jinsi ulivyochezwa, lakini hapakuwa na yeyote aliyekuwa tayari kumfunga paka kengele; kwani kuna kipindi ambapo Mkurugenzi wa Shughuli wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa [PCB] wa wakati huo, Edward Hosea, alikerwa na kutaka kuivalia njuga tafrani hii; lakini alivutwa shati na wakubwa wake, na hivyo Ikulu ikashauriwa “isipaniki”, kwa madai kwamba hapakuwa na ushahidi wowote juu ya vitendo vya rushwa katika mkataba huo.
Historia yajirudia kwenye rada
Historia kama hii imejirudia kwenye kashfa ya rada ambapo Serikali imedai kila mara kutokuwapo ushahidi juu ya ufisadi huo hadi tumeumbuliwa na jamii ya kimataifa kama tulivyoona mwanzo.
Inaelekea pia kwamba, hata kambi ya Upinzani nayo ilikuwa imelainishwa isipige kelele na kuuamsha umma juu ya sakata hili; kwani Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali wa wakati huo, Mheshimiwa John Momose Cheyo, hakupiga kelele kubwa juu ya jambo hilo.
Katika ushahidi uliotolewa katika ICSID, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati wa wakati huo, alidai kwamba alijaribiwa kwa rushwa ya dola 200,000 na mtu wa IPTL ili ailinde na kuitetea kampuni hiyo, lakini alikataa; na kwamba mtu huyo wa IPTL alimwachia kibahasha cha Sh. 500,000 nyumbani kwake siku ya Krismasi, 1994 wakati yeye hakuwepo nyumbani, lakini pia alimrudishia.
Naye Msaidizi wa Katibu Mkuu huyo, alitoa ushahidi kuthibitisha kwamba, alipewa kiasi hicho hicho cha fedha [dola 200,000] ili asaidie kutoa habari muhimu za mkuu wake wa kazi juu ya IPTL, ikiwezekana aweze “kushughulikiwa” kwa nguvu zote na kambi ya ufisadi nchini. [Alimtaja pia mtu mmoja katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetumwa kwake kumwahidi [yeye Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu], kwamba angepewa Shs. milioni 100m kama mradi wa IPTL ungepita [maelezo ya shahidi, 19 April 2000, uk. 3]. Hata hivyo, ushahidi huu ulikataliwa kwamba uliwasilishwa kwa kuchelewa.
Februari 2, 2001, mjini London, Mahakama hiyo ya Usuluhishi ya Kimataifa iliamua kwamba TANESCO [kupitia vigogo wa Serikali na TANESCO], ilikuwa na taarifa za kutosha juu ya kubadilishwa kinyemela kwa mitambo na IPTL kutoka SSD kuwa MSD kinyume na ile iliyokusudiwa kwenye mkataba kabla ya usimikaji kuanza. Na kwamba, kwa kuwa TANESCO hawakupinga hatua hiyo mapema, basi, walipashwa kujilaumu wenyewe.
Ni kwa sababu hii kesi ya TANESCO dhidi ya IPTL ilishindwa, na hivyo tukaamuriwa kulipa gharama za kesi na pia kuendelea kuilipa IPTL kwa miaka 20 ya mkataba.
Hatimaye IPTL ilianza kuzalisha umeme Januari 15, 2002 kwa asilimia 50, chini ya uwezo uliotajwa katika mkataba; huku TANESCO ikitakiwa kulipa zaidi ya dola milioni 4.6m kwa mwezi au dola milioni 55 kwa mwaka, kwa huduma na kwa kutumia umeme wa IPTL.
Chini ya mkataba huu, TANESCO [Serikali] inalipa dola milioni 3.6 [Shs. bilioni 5.4] kama ada ya huduma za mtambo [capacity charge] pekee kila mwezi. Juu ya malipo hayo, TANESCO inalipa senti 13 za Kimarekani kwa kila yuniti ya umeme kwa kuendesha mtambo kwa nusu ya uwezo wake [yuniti moja ni sawa na kilowati moja] kwa mwezi, na kufanya gharama zote kwa TANESCO kufikia zaidi ya Sh. bilioni kwa mwezi au Shs. bilioni 90 kwa mwaka.
Wananchi wabebeshwa zigo
Tunafahamu kwamba, TANESCO hawana fedha za kulipa malipo haya. Njia pekee kwa TANESCO ni kuongeza bei ya umeme kwa Watanzania masikini. Kwa mujibu wa gharama hizi, umeme wa IPTL unapashwa kuuzwa senti za Kimarekani 13 au Sh. 120 kwa yuniti ikilinganishwa na umeme rahisi wa Kidatu [hydro] wa senti 3 au Shs. 28 kwa yuniti.
Ni kwa sababu hii kwamba, serikali sasa inatoa ruzuku zaidi ya dola milioni 1.6. [Sh. 2.4] kwa TANESCO kila mwezi. Pamoja na hatua hiyo, bado mzigo kwa TANESCO ni mkubwa, na kwa vyovyote vile lazima bei ya umeme kwa mlaji iongezeke kati ya asilimia 15 na 35.
Ongezeko hili sio tu linamuumiza mtumiaji wa kawaida; bali pia linapunguza hamasa ya wawekezaji kutoka nje. Kwa nchi yetu, IPTL ni nyoka mwenye sumu kali aliye chini ya uvungu.
Mradi wa IPTL umerudisha nchi yetu hatua tatu nyuma katika juhudi za maendeleo, na kwa sababu hii; wawekezaji wa Malaysia na baadhi ya wanasiasa wetu waliohusika na ufisadi huu wanapaswa kuwajibishwa.
Niungane na Brian Cooksey katika mada yake The Power and the Vainglory [uk. 3] kwa kutaja tu kwamba, kama isingekuwa hujuma za IPTL/VIPEM, tayari Tanzania ingekuwa inavuna gesi yake ya asili na kuokoa mamilioni ya fedha za kigeni kutokana na kuagiza mafuta ya mitambo.
Vivyo hivyo, hasara kwa uchumi wa nchi kutokana na upungufu wa umeme tangu mwaka 1997 ingeepukika kama mradi wa Songas usingehujumiwa na “sakata” hili na mizengwe hii ya IPTL.
Baya zaidi ni kwamba, Watanzania wamebebeshwa gharama kubwa za umeme pamoja na deni kwa taifa ambalo fedha zake zimenufaisha wajanja wachache. Baadhi ya wajanja hao wangali pamoja nasi, wakiendelea kutumbua salama walichopora. Serikali inapofumbia macho ufisadi huu, wananchi waieleweje?

Wasomaji

334
Wasiliana
na mwandishi
Joseph Mihangwa
Barua pepe:
jmihangwa@yahoo.com
Simu:
+255-0713526972

Toa maoni yako!

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.
Copyright © 2011 Raia Mwema Newspaper Company unless othe

No comments:

Post a Comment