SAFARI ya kisiasa ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) mkoa wa Arusha James Millya, huenda ikafikia tamati ndani ya chama hicho baada ya Kamati ya Maadili na Kamati ya Siasa ya Mkoa “kumkaanga” kwa kupitisha maamuzi kuwa Mwenyekiti huyo anyang’anywe kadi yake na pia avuliwe nafasi zote za uongozi anazoshikilia.
Taarifa zilizolifikia Raia Mwema kutoka ndani ya vikao hivyo na baadaye kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa CCM zilizeleza kuwa baada ya kufanya mahojiano na wahusika wote, kamati ya maadili na ile ya siasa ya mkoa ilithibitisha pasipo shaka kuwa madai yanayotolewa na vijana hao hayana msingi zaidi ya kutumiwa na wanasiasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
Wajumbe wa Kamati ya Maadili waliosimamia mahojiano hayo ambao wanatoka makao ya makuu ya CCM Dar es Salaamni pamoja na Matson Chizii, Kanali Mhando, na wengine waliofahamika kwa jina moja moja la Mzee Malinda na Lipiko.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia mgogoro ulioibuka tangu mwezi Machi mwaka huu ndani ya Jumuiya hiyo ambapo kumekuwa na makundi mawili yanayopingana kuhusu vita inayoendelea ndani ya chama hicho inayohusiana na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM.
Kufuatia makundi ya vijana yanayolumbana, Millya kama Mwenyekiti na kiongozi wa juu, alimshambulia hadharani Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda akimtuhumuwa kuwa ni kiongozi asiyefaa na amehusika kukihujumu chama hicho kushindwa katika majimbo ya Arusha Mjini na Karatu kuchukuliwa na Upinzani katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana.
Aidha Mwenyekiti huyo pia anadaiwa kuwachochea vijana wa wilaya mbalimbali ambao wanadaiwa kulipwa fedha na kundi la viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya CCM kuandamana hadi ofisi za mkoa wakimtaka Chatanda aachie nafasi yake ya ukatibu kwa kuwa analipwa mishahara miwili kupitia ajira yake ya ubunge na ile ya ukatibu.
“Tuhuma zilizomgusa Millya ni pamoja na kuratibu maandamano haramu, kutoa lugha ya kichochezi dhidi ya Katibu wa CCM mkoa, kusema uongo na kuudanganya umma kuhusu mshahara wa Katibu”, alieleza mtoa habari wetu kutoka ndani ya vikao hivyo.
Uamuzi huo wa kumtosa Millya ambao ni moja ya kati ya maamuzi magumu kuwahi kufanywa na chama hicho mkoani kwa kipindi kirefu, ulifikiwa katika vikao vilivyofanyika kwa siku mbili mfululizo kati ya Jumamosi na Jumapili ya wiki iliyopita katika ofisi za chama hicho mkoa wa Arusha ambapo pia kamati hizo zimependekeza wanachama wengine wanane wa jumuiya hiyo ambao ni wafuasi wa Mwenyekiti huyo wa Vijana, nao wafukuzwe chamani.
Wanachama hao wa Jumuiya ya Vijana ambao wamekuwa wakiongoza harakati za kutaka Chatanda aondoke ni pamoja na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa UV-CCM Wilaya ya Arusha Mjini na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Ally Bananga, Fatma Ngairo, Philemon Ammo, Ally Majeshi na John Nyiti ambaye ni Katibu kutoka wilaya ya Arumeru.
Mtoa taarifa wetu anaeleza kuwa awali kamati ya maadili ilianza mahojiano na wanachama hao siku ya Jumamosi, na mtu wa kwanza kuhojiwa alikuwa Mwenyekiti wa Vijana (Millya) ambaye kamati ya maadili ilimtaka athibitishe madai yake kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, ni tatizo na mzigo kwa chama hicho.
“Awali Millya alikana taarifa hizo, lakini wajumbe walimwonyesha sehemu ya mkanda wa video uliorushwa kama taarifa ya habari na moja ya vituo vya televisheni nchini ambapo alirekodiwa akisema kuwa yeye ni mtumishi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoendesha kesi za mauaji ya Rwanda (ICTR), na kwamba Chatanda hafai hata kuwa mtumishi wake wa ndani (housegirl)”, alieleza mtoa taarifa wetu.
Wajumbe wa kamati walithibitisha baadaye kuwa Millya alidanganya umma kwani hakuwahi kufanya kazi katika mahakama hiyo, na kauli hiyo ililenga kumdhalilisha Chatanda mbele ya umma na haikupaswa kutolewa na kiongozi wa juu wa CCM, na hivyo alikuwa amevnja moja ya miiko mikuu ya chama hicho tawala.
Imeelezwa kuwa mbele ya kamati hiyo pia Millya alishindwa kuthibitisha kuwa madai yake kuwa Chatanda analipwa mishahara miwili kutokana na ajira zake mbili - ya ukatibu wa CCM anapokea mshahara wa Shilingi milioni 2 na ile ya ubunge ambayo anapokea mshahara wa Shilingi milioni 12.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa, hata hivyo, Millya alishindwa kuthibitisha madai hayo mbele ya kamati, na ili kuonyesha kuwa kamati haimwonei walitoa nyaraka za mshahara wa ubunge kutoka ofisi ya Bunge ambazo zilionyesha kuwa Chatanda anapokea mshahara wa Shilingi milioni 7; huku akiwa hajawahi kupokea mshahara wowote kutoka CCM tangu alipoteuliwa kuwa mbunge mwezi Novemba mwaka jana.
“Hapo ndipo Millya alipoanza kubaini kuwa mambo yanakwenda kombo kwa upande wa kambi yake, na baada ya mahojiano aliondoka eneo hilo kwa kutumia gari la kukodi; huku akiwa amesahau gari lake”, alieleza.
Aidha, kamati iliendelea kuwahoji wanachama wengine ambao walitoa madai mengi dhidi ya Chatanda na mjumbe wa Baraza la Vijana Taifa, Mrisho Gambo kwamba alipewa fedha kiasi cha Shilingi milioni 60 na mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne ambaye ana malengo ya kugombea urais mwaka 2015 kupitia CCM.
Hata taarifa zinaeleza kuwa baada ya kuwabana, vijana hao walishindwa kuthibitisha madai hayo mbele ya kamati ambayo ilibaini kuwa ni uzushi uliolenga kuchafuana kisiasa; hivyo kupitisha maamuzi kuwa vijana hao nao wanyang’anwe kadi za uanachama.
“Kamati pia ilibaini kuwa vijana hao wanatumiwa na baaadhi ya wanasiasa na hilo linathibitishwa na kauli iliyotolewa na mmoja wao mbele ya kamati kuwa “wako kibiashara zaidi” katika shughuli nyingi za kisiasa wanazoshiriki; kauli ambayo iliwashtua sana wanakamati, na hivyo kuamua kuwa waondolewe chamani”, aliendelea kueleza.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya kumaliza mahojiano ndipo ulipokuja wakati mgumu wa kupitisha maamuzi ambapo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole alitoa hoja ya kumtetea Millya kuwa apewe onyo kali badala ya uamuzi wa kuvuliwa nyadhifa zake.
Inaaminika kuwa Nangole na Millya wote wako katika mradi wa pamoja wa kumsafisha Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kutokana na tuhuma nyingi zinazoelekezwa kwake na wanachama na viongozi zinazohusiana na ufisadi. Millya amenukuliwa mara nyingi akiweka wazi msimamo wake kuwa “Lowassa kwanza CCM baadaye”.
Katika kujenga hoja, Nangole aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya Siasa, ambayo yeye ni Mwenyekiti, kuwa kwa kumfukuza Mwenyekiti huyo, Vijana wengi wangeasi dhidi ya CCM kwa kuwa ana wafusi wengi na anaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana.
Taarifa zinadai kuwa hoja hiyo ilipingwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Elisa Mollel (mbunge wa zamani wa Arumeru) ambaye aliwaeleza mwajumbe kuwa huu si muda wa kuwaogopa watu ndani ya chama; kwani CCM ni taasisi kubwa kuliko mtu yeyote na kuongeza kuwa ni lazima watangulize maslahi ya chama chao badala ya maslahi binafsi. Hoja hiyo iliungwa na wajumbe wengine wote.
“Kufuatia hoja ya Mwenyekiti, wajumbe walipendekeza ipigwe kura ya siri na matokeo yakaonyesha kuwa Millya alipata kura moja inayomtetea lakini wajumbe wengine walikubaliana na hoja na mapendekezo kuwa afukuzwe ndani ya chama”, alieleza mtoa habari huyo.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Onesmo Nangole alikataa kuthibitisha maamuzi yaliyofikiwa; huku akisema kuwa yaliyojadiliwa si maamuzi ya mwisho; kwani ni mapendekezo yatakayopelekwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa.
“Yaliyojadiliwa, kama desturi, ni siri ya chama lakini yatapelekwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kitakachofanyika muda wowote kuanzia sasa, na baada ya hapo mapendekezo hayo yatapelekwa kwenye vikao vya juu vya chama”, alisema.
Nangole alieleza kuwa pia Kamati ya Siasa ya Mkoa itawahoji vijana waliotoa tamko la kuwataja hadharani viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi ili kujua ukweli kuhusu aliyewatuma kutoa kauli hiyo na kwa maslahi ya nani.
“Hawa wamehojiwa na kamati ya maadili tu, lakini sisi kamati ya siasa pia tutawaita na kuwahoji kujua nani kawatuma na huyo mtu ana maslahi gani, na lengo letu sasa ni kusafisha Chama”, alisema.
Kuhusu madai ya kumtetea Millya ndani ya vikao, Mwenyekiti huyo wa CCM wa Mkoa aliyakanusha kwa kusema:”Hapana, hayo ni majungu tu. Sina haja ya kumtetea mtu yeyote. Kila aliyetuhumiwa ana uwezo wa kujitetea; kwani wote ni watu wenye uzoefu ndani ya chama”.
Naye Millya alipopigiwa simu yake iliita bila kujibiwa muda wote, lakini alikaririwa na gazeti moja la kila siku akieleza kuwa amepata taarifa za kuvuliwa madaraka yake na kusema kuwa mpango huo hauwezi kufanikiwa kwa sababu anawakilisha hisia na hoja za vijana wa CCM.
Aidha, taarifa zaidi kutoka ndani ya CCM zilieleza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kinatarajiwa kukutana Novemba 11, mwaka huu, katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Arusha, na tayari harakati za kumwokoa Millya na wenzake kuhakikisha kuwa mapendekezo ya kamati zote mbili yanapigwa “teke” zimeanza.
Habari zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali zilieleza kuwa tayari timu ya wajumbe 10 imeundwa ambao wameanza kazi ya kuzunguka kwa wajumbe wa halmashauri wa mkoa kutoka wilaya zote za mkoa wa Arusha ambazo ni Arusha Mjini, Karatu, Monduli, Arumeru na Longido ili kuwashawishi wajumbe wakatae mapendekezo yaliyotolewa na kamati zote mbili.
Akizungumza na Raia Mwema, mmoja wa wajumbe hao alijigamba kuwa mapendekezo hayo ‘yataozea’ kwenye majalada; kwani watahakikisha kuwa Halmashauri Kuu ya Mkoa inayazima mara moja na kati ya Jumanne na Jumatano walikuwa katika wilaya za Longido na Karatu wakitumia magari ya kukodi kwa kazi ya kuwashawishi wajumbe wa NEC Mkoa.
Na kama ilivyo kawaida na desturi iliyozoeleka katika vikao vya maamuzi ya CCM ya sasa, katika mpango huo tayari fungu kubwa la fedha limetengwa kwa ajili ya wajumbe watakaojenga hoja za kukataa maamuzi na mapendekezo ya kamati hizo kuhakikisha kuwa Millya anabakia na madaraka yake.
“Nakuambia tutapigana mpaka tone la mwisho la damu yetu lakini hakuna mtu atakayefukuzwa chamani, na sisi tumepanga mikakati ya nguvu na mapendekezo yote yatakosa maana katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Mkoa”, alisema mwanachama huyo.
Iwapo hatua ya kumvua Millya madaraka yake itafanikiwa, basi itakuwa pigo kubwa kwa kambi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye inadaiwa amekuwa akimtumia Millya katika harakati zake za kujijenga kisiasa baada ya kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri mkuu mwaka 2007 kutokana na kile kinachofahamika kama kashafa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Aidha, hatua hiyo pia itakuwa pigo kubwa na mwisho wake kisiasa kwa Millya mwenyewe ambaye kisiasa bado hajakomaa; kwani ni mara yake ya kwanza kushika nafasi ya juu katika uongozi wa CCM baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UV-CCM mwaka 2008.
No comments:
Post a Comment